Maonesho haya yanatafanyika kwa siku saba (7) katika Mkoa wa Morogoro kuanzia Tarehe 08/05/2022 mpaka Tarehe 14/05/2022.

Akizungumza katika mkutano wa Waandishi wa Habari Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’i Issa amesema maonesho hayo yatashirikisha Mikoa ya Kikanda ikiwemo Morogoro, Pwani Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

Katibu Mtendaji ametoa mwaliko kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa mingine kushiriki katika maonesho yatakayowakutanisha Wajasiriamali, Makampuni binafsi, Taasisi za Serikali na mashirika mbalimbali ya huduma za kijamii ili waweze kupata elimu na huduma mbalimbali zitakazotolewa.

Pamoja na mambo mengine, Bibi Beng’i ametoa shukrani zake kwa Mkoa wa Morogoro kwa mapokezi mazuri na ushirikiano wa dhati.

Kwa nafasi yake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigella amewataka wakazi wa Mkoa wa Morogoro ambao ndio wenyeji wa maonesho haya kujitoa kwa moyo na kutumia fursa hii kuinuka kiuchumi.

“Tuzalishe bidhaa kwa vingi vikiwemo vyakula na mahitaji mengine ili tunapopata ugeni huu tuwe tayari kutoa huduma na bidhaa zilizo bora” alisema Mhe. Shigella

Kwa namna ya pekee, Mkuu wa Mkoa amemkaribisha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kutangazwa kuwa mgeni rasmi wa siku ya kilele cha maonesho haya na amesisitiza kuwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro wana shauku kubwa ya kumuona pindi atakapokuja kuhitimisha maonesho hayo.

Kwa nafasi yake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuchochea kilimo Tanzania (TACT) Dtk. John Kyaruzi amesema wakiwa kama wadhamini wakuu wa maonesho hayo wako tayari na wamejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujifunza fursa mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kufanya maonesho hayo yenye Kauli Mbiu “Uchumi Imara kwa Maendeleo Endelevu” kuwa yenye faida na tija kwa Watanzania.