Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Sera wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB), Dkt.Nyankomo Marwa (wapili kulia) akibadilisha randama ya makubaliano na Katibu Mtendaji wa SAGCOT Kichocheo Bw.John Kyaruzi(wapili kushoto) yenye lengo la kuboresha mazingira ya upatikaji wa mikopo yenye tija kwa wakulima ili kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini. kushoto ni Mwanaseheria wa SAGCOT Kichocheo Bi.Ukundi Lema na Kulia ni Mkurugenzi wa fedha wa TADB Bw.Derick Lugemala

Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) imeingia makubaliano na Mfuko Kichocheo wa SAGCOT CTF kwa lengo la kushirikiana katika kuboresha mazingira ya upatikaji wa mikopo yenye tija kwa wakulima ili kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kusaini randama ya makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Sera wa Benki ya TADB, Dkt.Nyankomo Marwa alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambacho ni nguzo inayotegemewa kuchagiza maendeleo ya viwanda.

 “Kazi kubwa ya Benki ya Kilimo ni kuchachusha huduma za fedha katika sekta ya kilimo hivyo kupitia makubaliano haya yatasaidia zoezi la utoaji wa fedha kwenye miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo na mifugo,” alisema Dkt.Marwa.

Dkt.Marwa mbali ya kupongeza hatua iliyofikiwa, alisema mifumo ambayo imewekwa na SAGCOT – CTF itarahisisha zoezi zima la kuwafikia wakulima na hasa katika utoaji wa mikopo yenye lengo la kuijenga na kuimarisha sekta ya kilimo.

“Sisi kama Benki ya Kilimo tunalojukumu la kushirikiana na kufanya kazi na wadau mbalimbali katika sekta hii lengo likiwa ni kumkomboa mkulima na kuleta mageuzi ya kweli katika sekta hii muhimu katika uchumi wa Taifa,” alisema Dkt.Marwa.

Alisema hapo awali kuliwa na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wakulima na hasa wadogo ikiwemo kukopesheka na taasisi za kifedha lakini kuwepo kwa TADB kumeweza kutatua baadhi ya vikwazo vilivyokuwa vinarudisha nyuma ukuaji wa kilimo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa SAGCOT Kichocheo,Bw.John Kyaruzi alisema makubaliano hayo yatasaidia kufanikisha maboresho yanayoendelea katika sekta ya kilimo na kuleta unafuu kwa wakulima katika ngazi zote.

“Kama utakumbuka wakulima wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi hasa upatikanaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha na hata pale walipofanikiwa kupata mikopo hiyo riba yake ilikuwa kubwa na kurudisha nyuma maendeleo ya kilimo,” alisema Bw.Kyaruzi.

Bw.Kyaruzi alisema kuwepo kwa TADB na makubaliano ambayo wameingia yatakuwa ni mwarobaini kwa wakulima kunufaika na mikopo,” alisema na kuongeza kuwa makubaliano hayo yatakuwa na maana kubwa kwa wakulima.

“Sisi tunajihusisha na mambo makuu mawili ambayo kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika na kuwekeza kwenye miundombinu wezeshi kwa wakulima kuzalisha kwa wingi na kumfikia mlaji bila kikwazo chochote,” alisema.

Kwa mujibu wa Bw.Kyaruzi mfumo kichocheo haupo kwa ajili ya kushindana na taasisi za kifedha bali upo kwa ajili ya kuleta utengamano na kusaidia wakulima wanufaikie na huduma za kibenki kwa kupata mikopo yenye riba nafuu.

TADB kwa siku za hivi karibuni imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo na kuangalia namna bora ambayo inayoweza kuinua na kuimarisha shughuli za kilimo miongoni mwa wakulima hapa nchini.